Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kupitia kamati ya kituo cha Afya cha Mugango imesaini mikataba nane yenye thamani ya Shillingi Millioni 73,322,240 ambayo inajumisha kazi za ufyatuaji wa matofali na ujenzi wa majengo matano yanayotarajiwa kujengwa katika kituo cha Afya Mugango kilichopo Kata ya Mugango.
Zoezi hilo la utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa majengo ya upasuaji, kuhifadhia maiti, wodi ya kinamama, maabara, mtumishi na wafyatua matofali watatu lililohusisha kamati ya zahanati hiyo na wakandarasi (local fundi) limefanyika leo Ijumaa 21, Septemba 2018 katika ukumbi wa Zahanati hiyo uliopo Mugango.
Wakandarasi (local fundi) waliofanikiwa kupata kazi za ujenzi wa majengo hayo ni Ndg. Sylvanus A. Jairo atakayejenga jengo la kuhifadhia maiti, Ndg. Gideon Matto Egwaga atakayejenga jengo la wodi ya kinamama, Ndg. Hassan Ramadhan Magesa atakayejenga jengo la upasuaji, Ndg. Ernest Paschal Magige atakayejenga nyumba ya mtumishi na Yatanduka Co. Ltd itakayojenga jengo la maabara.
Sambamba na wakandarasi (local fundi) wa kujenga majengo hayo matano, waliofanikiwa kupata kazi ya kufyatua matofali yatakayotumika kwa ajili ujenzi huo ni Ndg. Paschal Nyagabona Anthon atakayefyatua matofali 6000, Ndg. Clifford James Nyamasagara atakayefyatua matofali 6000 na Ndg. Jumbula Macraud Rugola atayefyatua matofali 6500.
Ujenzi wa majengo hayo matano utakaotumia miezi minne tangu kuanza kwake 21, Septemba 2018 mpaka 19, January 2019 (kwa mujibu wa mkataba), utatumia njia ya kushirikisha wananchi katika kutekeleza mradi huo (force account).
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa manunuzi msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambaye pia ni katibu wa kamati ya manunuzi ya ujenzi huo Ndg. Joseph Chana Maitarya aliwataka mafundi hao kuhakikisha wanajenga majengo yenye ubora sambamba na kumaliza ujenzi huo kwa wakati.
"Wengi walijitokeza kuomba kazi ya ujenzi huu, ila nyinyi ndio mmekidhi vigezo, kati yenu kuna walioomba kujenga majengo matatu, mawili na wengine yote matano, lakini tumeona ni vyema kila jengo lijengwe na fundi msimamizi wa ujenzi mmoja ili kuongeza ufanisi sambamba na kumaliza kazi kwa wakati" alisema Maitarya.
"Kwa maana hiyo naomba mafundi mliopata kazi hii muhakikishe majengo mnayajenga katika ubora wa hali ya juu utakaoendana na makubalino tuliokubaliana katika mikataba mliyosaini, pia hakikisheni ujenzi unakamilika kwa wakati" alisema Maitarya.
Akizungumza kwa niaba ya mafundi waliopata kazi ya ujenzi wa majengo hayo na ufyatuaji matofali Ndg. Jumbula Macraud Rugola aliishukuru kamati ya kituo cha Afya Mugango na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg. John Lipesi Kayombo kwa kuendesha zoezi la kutafuta mafundi kwa uwazi na kwa weledi mkubwa sambamba na kupata kazi hizo.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma
Musoma Town opposite to Airport
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa