Tuesday 3rd, February 2026
@KIWANJA CHA SHULE YA AWALI NA MSINGI BWAI
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeanza rasmi leo, tarehe 26 Januari 2026, siku ya kwanza ya utekelezaji wa Kambi Maalum ya Huduma ya Kutatua Kero za Wananchi. Kambi hii itatekelezwa kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 26 hadi 28 Januari 2026 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Bwai, vilivyopo Kata ya Kiriba.
Lengo kuu la kambi hii ni kuwasikiliza wananchi, kupokea kero zao, na kuzitatua kwa kuwapatia huduma mbalimbali karibu na maeneo yao wanayoishi. Kupitia zoezi hili, Halmashauri inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa kuwakutanisha wananchi na taasisi za Serikali katika eneo moja kwa wakati mmoja.
Taasisi na idara mbalimbali za Serikali zimeweka matenti maalum kwa ajili ya kutoa huduma kulingana na majukumu yao. Wananchi wamejitokeza kwa wingi na wanaendelea kujitokeza katika matenti hayo ili kupata huduma, ushauri, na ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika sekta mbalimbali.
Mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya Kambi Maalum ya Huduma ya Kutatua Kero za Wananchi ni Mheshimiwa Juma Chikoka, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, ambaye amefungua rasmi zoezi hilo kwa kutembelea mabanda mbalimbali ya huduma kutoka taasisi na idara za Serikali zikiwemo TRA, TANESCO, NIDA, RITA, NIC, Sekta ya Madini, pamoja na idara za Afya, Elimu, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii, Dawati la Jinsia, RUWASA, MUWASA, Biashara, Mapato, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Damu Salama, Huduma za HIV, Lishe, Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa Yanayoambukiza, Uzazi wa Mpango, Ardhi, TARURA na nyinginezo.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika siku zote tatu za kambi hii ili kunufaika na huduma zinazotolewa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa