Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imetembelea na kukagua athari za kimazingira na kijamii zinazoweza kuletwa na mradi wa uchimbaji na uchenjuaji (processing) madini aina ya dhahabu wa Jema Partners.
Zoezi hilo la ukaguzi wa mradi huo unaotumia mfumo wa kutenganisha dhahabu kwa kutumia Cyanide (Vat leaching) katika hatua ya uchenjuaji (Processing) uliopo katika Kijiji cha Kaburabura, Kata ya Bugoji limefanyika jana Jumanne 11, Septemba 2018.
Mradi huo uliopo katika hatua za mwisho za kufunguliwa ni moja kati ya miradi ya uchimbaji wa madini aina ya dhahabu iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Afisa Afya na Mazingira wa Halmashauri hiyo Ndg. Mwizarubi E. Nyaindi alimtaka mwekezaji wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha vitu vilivyobaki kabla ya kuufungua mradi huo.
"Tumeangalia athari za kimazingira zinazoweza kuletwa na mradi huu, tumeona kwa kiasi kikubwa mwekezaji ameweza kudhibiti hilo" alisema Nyaindi.
"Kwa kiasi kikubwa mwekezaji amekamilisha matakwa ya kuanzisha mradi, kuna vitu vichache inabidi akamilishe kabla ya kuufungua mradi huu na akishakamilisha hivyo tutarudi tena kuja kukagua" alisema Nyaindi.
Mwisho Ndugu Nyaindi alimtaka Mwekezaji huyo kufika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili kuweza kupata ushauri, maelekezo na taratibu za ulipaji kodi na maswala ya kitaalamu juu ya uendeshaji wa mradi huo.
Imetolewa na
Kitengo cha habari na uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma
Musoma Town opposite to Airport
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa