Timu ya Wataalam kutoka Mkoani leo tarehe 14 Januari, 2026 imeanza rasmi zoezi la ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, zoezi lililoanza kwa kufanyika kwa kikao cha ufunguzi (Entrance Meeting).
Kikao hicho muhimu kiliwakutanisha Wataalam wa Mkoa pamoja na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, ambapo pamoja na mambo mengine, wajumbe walijadili madhumuni ya ufuatiliaji wa miradi, upeo wa zoezi hilo, pamoja na kuweka mikakati ya ushirikiano katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi, ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Baada ya kikao hicho, Timu ya Wataalam wa Mkoa kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ilianza kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo. Katika ziara hizo, timu ilifanya ukaguzi wa kina kwa kujionea hatua za utekelezaji wa miradi, kukagua ubora wa kazi zinazofanyika, pamoja na kutathmini matumizi ya fedha ili kuhakikisha kuna thamani halisi ya fedha zilizotolewa (Value for Money).
Aidha, wataalam walipata fursa ya kuzungumza na wasimamizi wa miradi, wakandarasi pamoja na kamati za wananchi, ambapo walipokea maelezo ya utekelezaji wa miradi na kubaini changamoto mbalimbali zilizopo. Kupitia ukaguzi huo, Timu ya Wataalam wa Mkoa ilitoa ushauri wa kitaalam na maelekezo ya awali yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa miradi, kuondoa mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeeleza kuendelea kushirikiana kikamilifu na Timu ya Wataalam wa Mkoa katika zoezi hilo, huku ikisisitiza dhamira yake ya kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na tija, kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo endelevu kwa wananchi.
Zoezi la ufuatiliaji wa miradi linaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika ipasavyo na miradi inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa Wilaya ya Musoma.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa