Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamewasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la One Stop Center katika Mwalo wa Busekera, uliopo Kata ya Bukumi.
Kabla ya kuelekea eneo la mradi Busekera, wataalamu hao walipata wasaa wa kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Juma Chikoka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mhe. Maregesi Samweli pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Ndugu Palela. Katika kikao hicho, viongozi hao walipata fursa ya kubadilishana taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi, malengo yake, pamoja na mchango wake katika kuboresha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Musoma.
Ziara hiyo imelenga kukagua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, kuhakikisha ujenzi unazingatia viwango, taratibu na michoro iliyopitishwa, pamoja na kutathmini utayari wa kituo hicho katika kurahisisha utoaji wa huduma za sekta ya mifugo na uvuvi.
Ujenzi wa One Stop Center katika Mwalo wa Busekera unatarajiwa kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi, kurahisisha huduma kwa wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Kata ya Bukumi na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa