1.0 UTANGULIZI:
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ni moja kati ya Halmashauri tisa (09) za Mkoa wa Mara, ilisimikwa rasmi kama Halmashauri mwaka 1984 chini ya kifungu cha 4 cha sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 333.
1.2 ENEO
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ina jumla ya eneo la Kilometa za mraba 2,652.87 (Nchi kavu ni 2,455.87 Km2 na Majini 197 Km2). Umbile la Halmashauri kiujumla ni tambarare likiwa na vilima vidogo vya mtawanyiko. Halmashauri ipo kusini mashariki mwa ziwa Victoria kati ya nyuzi 1°30’ za Latidudo na Latitudo nyuzi 2°00’ kusini mwa Ikweta Aidha, Halmashauri ipo nyuzi 32°15’na nyuzi 30° Longitudo Mashariki ya mstari wa Grinwichi.
1.2.1 MIPAKA
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma inapakana na Manispaa ya Musoma kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Butiama kwa upande wa Mashariki, Ziwa Victoria upande wa Kusini na Wilaya ya Bunda upande wa kusini mashariki na Ziwa Victoria upande wa Magharibi.
1.2.2 HALI YA HEWA
Halmashauri ipo kwenye mwinuko wa mita 1,500 kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha juu cha joto kwa mwaka ni Nyuzi joto kati ya 240C na 320C na kiwango cha chini ni Nyuzi joto kati ya 200C na 240C, kiwango cha mvua ni kati ya 900mm na 1,200mm kwa mwaka, zinazoanza mwezi Oktoba hadi Desemba kwa mvua za vuli na mwezi Machi hadi Mei kwa mvua za masika.
1.3 IDADI YA WATU
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka 2022, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ilikuwa na jumla ya watu 266,665 ambapo kati ya hao, Wanaume ni 131,246 sawa na 49% na Wanawake ni 135,419 sawa na 51%. Ongezeko la watu katika Halmashauri ya wilaya ya Musoma limefikia asilimia 2.1 kutoka mwaka 2012 mpaka 2022. Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wastani wa pato la Mwananchi kwa mwaka ni Shilingi 2,377,992.01 kwa mwaka.
1.4 HALI YA UCHUMI YA HALMASHAURI YA WILAYA
Shughuli kuu ya kiuchumi kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ni Uvuvi ambayo huajiri asilimia 85 ya wakazi wote, shughuli nyingine za uchumi ni Kilimo, (5%), Ufugaji (5%), madini (2%) na shughuli nyingine zilizobaki huajiri asilimia 3 ya wakazi. Mazao yanayolimwa ni Alizeti, Ulezi, Muhogo, Mtama na Viazi. Ziada ya Mazao haya ya chakula hutumika kwa biashara. Aidha shughuli za biashara ndogondogo ni ajira mbadala zinazochangia katika pato la wakazi wa Halmashauri ya Musoma.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa