Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg.Msongela Palela Leo Novemba 13, 2025 katika ukumbi wa Makanya uliopo Kata ya Mugango Kijiji cha Kwibara amefanya kikao na wakuu wa shule za sekondari na Msingi,Wenyeviti wa vijiji na Vitongoji, Watumishi ngazi ya vijiji na Kata Pamoja na viongozi ngazi ya Halmashauri kwa dhumuni la kuboresha utendaji katika vijiji vyetu hasa utoaji wa elimu bora
“Serikali zetu za vijiji zimejipangaje katika zoezi la utoaji wa chakula shuleni?” Ameuliza Mkurugenzi Msongela ambapo Ndg. Richard Charles ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Bulinga amesema sababu kubwa ya wazazi kutochangia chakula cha wanafunzi mashuleni ni matumizi mabaya ya vyakula hivyo kwani vinatumiwa na walimu badala ya wanafunzi na hivyo hawaoni umuhimu wa kuchangia chakula. Sambamba na hilo amesema kuwa ubora wa chakula kinachotolewa shuleni ni mdogo hivyo kupelekea chakula hicho kutoliwa na Watoto wao hivyo hawaoni haja ya kuchangia chakula ambacho Watoto wao hawakitumii
Ndg.Msongela amesisitiza jamii zetu kushiriki katika utoaji wa chakula shuleni kwani chakula ni hitaji la msingi na sio anasa na mtoto mwenye njaa hawezi kusoma.Tunapochangia chakula, tunachangia afya,mahudhurio na mafanikio ya wanafunzi wetu. Ndg. Msongela ameahidi ubora na usalama wa chakula hicho. “Tunaandaa kinyago ambacho kwa kila kata itakayokuwa ya mwisho katika zoezi hili itakichukua na kukaa nacho kwa mwaka mzima ila kwa Kata itakayofanya vizuri nayo itazawadiwa”. Amesisitiza Mkurugenzi
Aidha Utoro shuleni umekithiri katika maeneo yetu. Sisi kama viongozi tunatumia mikakati gani katika kukomesha utoro shuleni?.Kadri tunavyokwenda ndivyo utoro unavyozidi,sasa hawa Watoto wanakwenda wapi? Yawezekana hawa ndio wanaotusumbua huko!
Wakijibu hoja hizo zilizotolewa na Ndg.Palela, wajumbe wa kikao wamesema sababu zinazopelekea utoro shuleni ni Pamoja na mimba za utotoni,uvuvi,ufugaji,uchimbaji madini,mdondoko wa wanafunzi na baadhi ya Watoto kuwa wakuu wa kaya
“Kuanzia leo nawaagiza walimu wakuu na Maafisa elimu Kata kuhakikisha orodha ya watoro inapelekwa kwenye WDC kwa majadiliano. WEO, VEO na Mwenyekiti wa Kijiji wafuatilie kila mwanafunzi mtoro.Kila WEO ahakikishe anawasilisha ofisi ya Mkurugenzi orodha ya wanafunzi waliorejea shuleni wiki ya kwanza ya Januari ,2026 shule zitakapofunguliwa.” Amesisitiza Ndg. Msongela
Aidha, Usalama wa watumishi wanaokuja katika maeneno yetu umeshuka kutokana na watumishi hasa walimu wakishambuliwa,kuuawa na wengine kuibiwa mali zao. Tunatoa wito kwa serikali za vijiji na Kata kuhakikisha walimu wanalindwa,wanaheshimiwa na wanapata mazingira salama ya kufundishia. “Nakemea tabia ya watumishi wa serikali kuwashambulia Wenyeviti wa Vijiji Pamoja na vitongoji kwani kwa kufanya hivyo ni kuwakosea adabu.sisi ni wamoja hivyo inabidi tufanye kazi kwa kushirikiana” . Amesisitiza Mkurugenzi Palela
Ndg. Palela amesisitiza Uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza,MEMKWA, darasa la kwanza na awali kwa mwaka 2026 uanze mara moja. Ifikapo Desemba 31,2025 uandikishaji uwe umekamilika ili wanafunzi waanze masomo kwa wakati. Wenyeviti tuna jukumu la kuhakikisha Watoto wetu wote wanaandikishwa kutokana na changamoto ya jamii tuliyonayo kwa wazazi kutoridhia Watoto wao waende shuleni. Wanafunzi wote lazima waandikishwe na kuhudhulia shuleni haijalishi kama ana sare ya shule au hana ili tupate ufumbuzi wake. Lazima sisi wenyeviti tuunge mkono serikali yetu kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanaenda shule
Naomba taarifa tunazotoa kutoka katika maeneo yetu ziwe sahihi na za kweli kwani kumekuwa na tabia ya kutoa taarifa zisizo za kweli na kupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi katika maeneo yetu kutokana na taarifa hizo.Pia tuangalie namna ya kutenga maeneo yetu kwa ajili ya shughuli mbalimbali za miradi ya serikali kama ujenzi wa shule Pamoja na Zahanati.Fedha za miradi zinapoletwa na serikali katika maeneo yetu ila sisi watendaji kwa ngazi ya vijiji tunaendelea kuvutana kuhusu maeneo ya miradi hii. Ni lazima tufanye maamuzi sasa ya kutenga maeneo ya miradi ili kujilidhisha na maeneo hayo na kama itawezekana kuyatafutia hati miliki ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa