Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoani Mara limegomea ongezeko la shilingi 100 katika kila kilo ya samaki ambayo ilipendekezwa kuongezeka ili ifikie 200 katika bei ya sasa iliyopo ya Shilingi 100 kwa kilo.
Uamzi huo, umefanywa na Madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao cha baraza hilo robo ya tatu kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa katoliki uliopo Kata ya Mugango Wilayani ya Musoma.
Pendekezo hilo la ongezeko la tozo ya shilingi 100 liliwasilishwa na kamati ya fedha na mipango katika baraza hilo na ndipo madiwani walipopata fursa ya kujadili na wengi wao walisema kwa sasa hakuna haja ya kuongeza tozo badala yake shilingi 100 inayotozwa iendelee kutozwa kuwapa ahueni wafanyabiashara wa samaki na wananchi kwa ujumla.
Diwani wa kata ya Nyakatende Wilaya ya Musoma Mhe. Malele John alisema kuwa iwapo baraza hilo litaridhia ongezeko hilo wananchi na wafanyabiashara wa samaki wataumia. Hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kulipa shilingi 100.
"Hoja ya ongezeko la tozo shilingi 100 itasababisha Wafanyabiashara ambao kwa sasa wanalipa tozo waache na badala yake utoroshaji wa samaki utashamili. Hoja sio ongezeko la tozo bali usimamizi madhubuti ufanywe na(management) Halmashauri ." Tukiongeza tozo hii eti walipe 200 kwa kila kilo tutawaumiza wananchi wetu." alisema Mhe. Shimiwa John.
Diwani wa kata ya Etaro Mhe. Emmanuel Majiga alisema bei ya samaki imekuwa ikishuka mara kwa mara katika soko la dunia. Kitendo cha kuongeza tozo ni kuwapa tabu wananchi.
"Sioni sababu ya kuongeza mzigo wa tozo kama huko nyuma tulishindwa kutoza shilingi 250 iliyokuwepo tukaitoa baada ya kushindwa kuleta ufanisi. Tuendelee kutoza tozo iliyopo na pia vyanzo vingine vya mapato ikiwemo migodi na masoko isaidie kuongeza mapato ya halmashauri yetu sio kujikita katika chanzo hiki pekee cha tozo ya samaki." amesema Jogoro malyango diwani kata ya Suguti.
Nae Diwani wa kata ya Bulinga Abel Mafuru ameiomba halmashauri hiyo kuangalia upya kuhusu suala la leseni za mitubwi pamoja na maegesho ya mitumbwi ambapo amesema leseni moja ya mtumbwi ni si chini ya shilingi laki moja na elfu thelasini na nane
" wavuvi wanamakato makubwa leseni tu ya mtubwi katika halmashauri yetu, mtubwi wa kasia ni shilingi 115,000 huku mtubwi wa mashine ni shilingi 138'000 bei ya leseni hizi ziko juu tofauti na wilaya nyingine, maegesho ya mtumbwi nayo ni shilingi 15000 kwa mtumbwi moja kwa mwezi hivyo kuongezeka kwa tozo ya kilo ya samaki ni kumuumiza mvuvi" alisema Abel Mafuru Diwani kata ya Bulinga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Charles Magoma amesema suala hilo lirudi tena katika menejimenti na kulichakata upya na kuja na mapendekezo mapya ambayo yatakayo shawishi baraza hilo kuona haja ya ongezeko hilo, huku Mkuu wa Wilaya akiwasihi madiwani hao kuona haja ya uwepo wa ongezeko hilo la tozo ya samaki kwani ndio chanzo kikuu cha mapata katika Halmashauri hiyo.
"Niombe Mkurugenzi mkachakate upya jambo hilo kwani zamani tulitoza shilingi 250 kwa kilo ya samaki lakini ilileta shida kweli hivyo mkachakate na kuona mzani unawezaje kuwa sawa" alisema Charles Magoma Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma.
" Msingi wa ongezeko hilo la tozo ni kuongeza makusanyo ya ndani ambapo katika Halmashauri nyingine kama Bunda na Musoma Manispaa wanatoza kilo ya samaki kwa shilingi 300 lakini Halmashauri yetu tupo chini kwa kutoza shilingi 100 kwa kilo" alisema Dk. Halfan Hauled mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Nae Kaimu Mkurugenzi Ndg. Magange Mwita wa Halmashauri hiyo alitolea ufafanuzi wa hoja ya ongezeko la tozo hiyo kuwa ni baada ya mapitio ya bajeti .Halmashauri imeingia kwenye makisio ya makusanyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 ya shilingi Bilioni 1.9 ambapo awali makusanyo ya bajeti kwa vyanzo vya ndani yalikuwa ni shilingi Bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Musoma Town opposite to Airport
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa