Kampuni ya Polygold, inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, imechangia jumla ya madawati 300 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Shule za Awali na Msingi Kigera na Kigera B, zilizopo Kata ya Nyakatende, Kijiji cha Kigera.
Katika mgawanyo wa madawati hayo, Shule ya Msingi Kigera imepokea madawati 150, huku Shule ya Msingi Kigera B ikipokea madawati 150.
Hafla ya makabidhiano ya madawati hayo ilifanyika katika kijiji cha Kigera, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka. Katika hotuba yake, Mhe. Chikoka aliipongeza Kampuni ya Polygold kwa mchango huo mkubwa unaoonesha uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), hususan katika sekta ya elimu ambayo ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Aidha, Mhe. Chikoka aliwahimiza wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa Kampuni ya Polygold kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii, ikiwemo uhaba wa miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Ndg. Msongela Nitu Palela, alishukuru kwa niaba ya Halmashauri na wananchi wa Kigera kwa mchango huo, akieleza kuwa madawati hayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za Kigera na Kigera B.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wananchi wa Kata ya Nyakatende, wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, watumishi wa Shule ya Awali na Msingi Kigera na Kigera B, pamoja na wadau mbalimbali kutoka Kampuni ya Polygold.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma inaendelea kuwakaribisha wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa