Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imetoa jumla ya shilingi milioni 135,420,000 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 11, ikihusisha vikundi 05 vya wanawake, 03 vya vijana na 03 vya watu wenye ulemavu, katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo hiyo.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo isiyo na riba iliyofanyika tarehe 09 Januari, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Charles Magoma, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Ndugu Majidu Mudrikat Kalugendo, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa sauti na nguzo kubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri kwa mujibu wa sheria.
Kalugendo amesema kuwa jukumu kubwa kwa sasa ni kurahisisha utoaji wa mikopo hiyo na kuhakikisha waombaji hawapati changamoto, huku Halmashauri ikijipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kuunda vikundi, kuomba mikopo, pamoja na kuhakikisha urejeshaji unafanyika kwa ufanisi.
“Hatua hizi ni sehemu ya kuhakikisha tunatimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri,” amesisitiza Kalugendo.
Aidha, amewatoa hofu wananchi kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo kwa kusisitiza kuwa fedha zipo na zitawafikia wanufaika wote waliokidhi vigezo, ambapo mikopo hiyo inatarajiwa kuchangia kuongeza kipato cha familia na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mikopo hiyo itatolewa kupitia mfumo wa kibenki, ambapo Benki ya NMB na Benki ya CRDB zimepewa jukumu la kusimamia utoaji wa fedha kwa vikundi vilivyoidhinishwa. Mfumo huu unalenga kuhakikisha uwazi, usalama wa fedha, pamoja na ufuatiliaji mzuri wa urejeshaji wa mikopo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa