Thursday 8th, January 2026
@KIJIJI CHA SUGUTI NA KIJIJI CHA BUSEKERA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewataka wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa nyingi zilizopo katika tasnia ya ufugaji wa samaki nchini, hususan ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Balozi Dkt. Bashiru ametoa wito huo Desemba 22, 2025, wakati wa ziara yake Wilayani Musoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, ambapo alifika Kijiji cha Suguti, Kata ya Suguti, kukutana na wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za ufugaji.
Akiwa Suguti, Waziri amehimiza wawekezaji wa ndani kuelekeza nguvu zao katika uanzishaji wa viwanda vya chakula cha samaki, uzalishaji wa vifaranga vya samaki pamoja na utoaji wa mikopo kwa vikundi vinavyojihusisha na ufugaji wa samaki, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina tija kubwa kiuchumi.
“Ufugaji wa samaki ni utajiri. Pamoja na changamoto zilizopo, wafugaji wengi wanaendelea na shughuli hii kwa sababu ya faida inayopatikana. Tunawakaribisha wawekezaji wa ndani hususan katika eneo la uzalishaji wa vifaranga ili kuhakikisha vinapatikana kwa wakati wote,” amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Baada ya hapo, Waziri alitembelea wavuvi wa samaki katika Kijiji cha Busekela, Kata ya Bukumi, ambapo alisikiliza changamoto zinazowakabili wavuvi hao na kuahidi Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uvuvi ili kuongeza tija na kipato kwa wananchi.
Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa tasnia ya ufugaji wa samaki ni miongoni mwa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaliyolenga kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi, hivyo amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa zilizopo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amesema wanawake na vijana wanaojihusisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wameanza kunufaika na programu hiyo, huku Serikali ikiendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza. Mmoja wa wanufaika amesema wafugaji waliopata mikopo ya vizimba awamu ya kwanza waliweza kuvuna samaki wengi na kurejesha mikopo yao licha ya changamoto za awali na Ziara hiyo imeendelea Wilayani Bunda
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa