Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka, leo tarehe 14 Januari, 2026, amefunga rasmi mafunzo ya Waheshimiwa Madiwani yaliyodumu kwa siku tatu, na kutoa maelekezo muhimu yanayolenga kuimarisha utendaji kazi na kuharakisha maendeleo katika Halmashauri.
Katika hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Chikoka amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kujiepusha na migogoro isiyo na tija inayoweza kuzorotesha kasi ya maendeleo katika Halmashauri hizo.
Amesisitiza kuwa migogoro yote isiyo na manufaa haipaswi kupewa nafasi, huku akiwataka Madiwani kudumisha ushirikiano mzuri kati yao na Timu za Wataalam katika Halmashauri husika ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi.
Mhe. Chikoka ameongeza kuwa Serikali haitarajii kuona baada ya mafunzo hayo Madiwani wakivuka mipaka ya mamlaka yao, bali watumie mafunzo hayo kama fursa ya kuweka mikakati thabiti ya kuleta mabadiliko chanya katika uongozi wao na kuacha alama itakayodumu kwa manufaa ya wananchi.
“Twende tukaache alama katika nafasi zetu tunazozitumikia” amesisitiza Mhe. Chikoka.
Aidha, ameeleza kuwa wananchi wanahitaji maendeleo ya haraka, hivyo ni muhimu kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha na ubora wa kazi zinazotekelezwa.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa hili ni suala la kufa au kupona, na litakuwa ajenda ya kudumu kwa wadau wote wa maendeleo ndani ya Halmashauri.
Mafunzo hayo ya Madiwani yalilenga kuwajengea uwezo, kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwajibikaji na tija inayotarajiwa na wananchi wa Wilaya ya Musoma.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Suguti - Kwikonero, Barabara ya Majita) | 31117 - MUSOMA.
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa