Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji imeanza mpango wa kupeleka maji katika vijiji 31 vinavyozungukwa na Ziwa Victoria, vilivyopo katika Halmashauri hiyo.
Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Busekera, Buira na Bukumi vilivyopo Kata ya Bukumi, Kastam Kata ya Bukima, Buanga na Rusoli Kata ya Rusoli, Musanja Kata ya Musanja, Bugwema, Masinono na Kinyang'erere Kata ya Bugwema, Murangi na Lyasembe Kata ya Murangi, Kasoma, Chumwi na Kaboni Kata ya Nyamrandirira, Tegeruka Kata ya Tegeruka, Maneke, Mwiringo na Kwikuba Kata ya Busambara, Kiriba, Bwai Kwitururu na Bwai Kumsoma Kata ya Kiriba, Kiemba na Kabegi Kata ya Ifulifu, Kigera Etuma/ Kakisheri Kata ya Nyakatende, Kurukerege na Mkirira Kata ya Nyegina, Kisiwa cha Rukuba, Mmahare, Busamba na Etaro Kata ya Etaro,
Mradi huo wa serikali wa kusambaza maji katika vijiji vinavyozunguka katika maziwa makuu ambayo ni Ziwa Victoria, Tanganyika na Rukwa umeingia katika awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza mwaka 2006 - 2015.
Mradi huo unaojulikana kwa jina là Programu ya uendelezaji wa sekta ya Maji awamu ya pili (WSDP II) umepangwa kuzunguka katika Mikoa mitano, Wilaya 19 na Vijiji 271.
Mikoa itakayonufaika na mradi huo ni Mara, Mwanza, Kagera, Simiyu na Geita.
Akizungumza wakati wa kikao kati ya wataalamu wa maji na wananchi wa kijiji cha Bwai Kwitururu kilichopo Kata ya Kiriba, mtaalamu wa Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Grayson Mdemu alisema mradi huo hakuna mwanakiji atakayelipwa fidia kwa kuwa mradi huo hautobomoa Nyumba ya mtu.
"Mradi huu utagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna mwananchi atakayelipwa fidia kutokana na mabomba kupita katika maeneo yenu, kwa kuwa hatutobomoa nyumba ya mtu yoyote kupitisha mabomba hayo" alisema Mhandisi Mdemu.
"Mradi huu una faida kuu tatu kuleta maji safi na salama kwa wananchi (Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 - 2020 ibara ya 55 kipengele A, kuboresha afya za wananchi na kuinua hali za uchumi" .
Wakati huo Mhandisi wa Maji Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mhandisi Emmanuel Masanja aliwataka wananchi wa vijiji hivyo 31 kuutunza na kuulinda mradi huo kipindi utakapoanza.
"Serikali imeamua kutuletea mradi wa maji katika vijiji 31 vilivyopo katika Halmashauri yetu, hii ni bahati na inatupasa kuulinda na kuutunza utakapoanza mradi huo " alisema Mhandisi Masanja.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Musoma Town opposite to Airport
Sanduku la Posta: P.o. Box 344 Musoma
Simu: 0282622163
simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@musomadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Haki zote zimehifadhiwa